SERIKALI ya awamu ya nne iliingia madarakani na kauli mbiu ya
“Maisha bora kwa kila Mtanzania.” Timu ya wana mtandao iliyoiingiza hii
serikali ndani ya ikulu yetu, ilibobea katika uundaji wa kauli mbiu.
Itakumbukwa kuwa ni timu hiihii ya wana-mtandao iliyoibuka na kauli
mbiu ya “Kasi mpya, Ari mpya na Nguvu mpya.” Hata baada ya mtandao
kusambaratika, Rais Kikwete na mtandao masalia walikuja na kauli mbiu ya
“Kasi zaidi, Ari zaidi na Nguvu zaidi.” Laiti mvuto wa kauli mbiu
ungeendana na uhalisia; Watanzania tungekuwa mbali sana.
Watu wengi hivi sasa wanakubaliana pasipo kutumia vigezo maalum
kuwa, chini ya serikali ya awamu ya nne, hali mbaya imekuwa na kasi, ari
na nguvu zaidi kuliko mambo mazuri.
Tamko hili bila vigezo linaweza kuonekana ni propaganda za kisiasa,
lakini kwangu mimi kigezo kikuu ni waasisi wenyewe wa kauli mbiu hizi
ambao nimeongea nao na wao wakakiri kuwa, “Mambo yamegeuka kinyume na
walivyotarajia.”
Hata ukitumia kipengele kimoja tu cha thamani ya shilingi ya
Tanzania ambacho ni mhimili mkuu wa shughuli zote za kiuchumi ndani ya
nchi, ni rahisi kuona ukweli wa hoja yangu.
Wakati serikali hii inaingia madarakani mwaka 2005, thamani ya
shilingi dhidi ya dola ilikuwa kati ya Sh. 1,000 na 1,100. Hivi sasa
shilingi imeporomoka sana na muda si mrefu yaweza kuingia shilingi
2,000 kwa dola moja hata kabla ya mwisho wa mwaka huu; huku mfumoko wa
bei ukipaa.
Kutokana na kuporomoka kwa thamani ya shilingi, wiki hii
tumeshuhudia matangazo ya kiama kwa Watanzania. TANESCO wametangaza
ongezeko la bei ya umeme wakati hata mgawo wenyewe haujaisha.
Mamlaka ya Udhibiti Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza
ongezeko la bei ya mafuta ya taa, petroli na dizeli. Ongezeko la bei ya
mafuta linakuja wakati ambapo hata baadhi ya vituo vya mafuta vilikuwa
bado vikiendelea na mgomo wa kuuza nishati hiyo. Ongezeko hili
halitegemewi kuondoa mgomo huo kwa sababu linatokana na kuporomoka kwa
thamani ya shilingi.
Inaeleweka vema kuwa ongezeko la bei ya umeme na mafuta linaongeza
moja kwa moja bei za bidhaa nyinginezo pamoja na huduma muhimu za
kijamii. Haitarajiwi kuwa ongezeko hili litaongeza ubora wa huduma wala
kuzisogeza karibu na watumiaji. Kimantiki, ongezeko la bei kwa huduma
hizi, ni ongezeko la maumivu kwa watumiaji.
Kama nilivyodokeza hapo juu, mtiririko wa matukio yanayofanya
maisha ya Watanzania kuwa magumu, ni kinyume na matarajio ya
wahandisi/wajenzi wa mfumo wa utawala wa serikali ya sasa. Hata wao
wanashangaa ni kwa nini mambo yanazidi kuwa magumu. Kinachokosekana ni
tamko lao hadharani kuwa hali ni ngumu.
Wanasema na kusononeka mafichoni wakati Watanzania waliowaweka
madarakani wanazidi kuumia. Kwa hali ya uchumi kugeuka na kuwa kinyume
na matarajio ni jambo la kawaida katika mifumo ya uchumi.
Kilicho kigeni katika hali yetu, ni tabia ya watawala kushindwa
kueleza wazi ni nini kimetokea na kufanya hali za Watanzania kuzidi kuwa
mbaya kuliko zilivyokuwa kabla hawajaingia madarakani. Badala ya
kusema ukweli, watawala wamekazana kutangaza kuwa uchumi unapaa na hali
ya Watanzania ni bora!
Kwa sasa kauli mbiu inayofaa ni ile ya “Maisha mabaya kwa kila
Mtanzania.” Haiwezekani kwamba watawala wetu hawa walikaa, wakapanga
kuwa walete maisha mbaya kwa kila Mtanzania. Lakini kutokana na kimya
chao, hisia zinaanza kujengeka miongoni mwa Watanzania kuwa yawezekana
walipanga hivyo. Hisia hizi zikiachwa ziaminike, itakuwa vigumu
kudhibiti ghadhabu ya wananchi dhidi ya serikali hii.
Awamu iliyopita ilikabidhi mustakabali wa uchumi wa taifa letu
mikononi mwa wawekezaji. Serikali iliuza kila kitu na kufungua milango
yote kwa wawekezaji. Matokeo ya sera hii, wote tumeyaona kwa masikitiko
makubwa sana.
Watanzania wamegeuka kuwa wapangaji na wapagazi huku wageni wakiwa
wamiliki wa njia kuu za uchumi. Rais Mkapa aliwahi kunukuliwa
akisikitika kuwa hali hii hakuikusudia kwa sababu alidai yeye alilenga
“kubinafsisha” siyo “kubinafasisha.”
Chini ya serikali ya Mkapa, wawekezaji walipata ushirikiano mzuri
wa serikali na kuwekewa mazingira ya kunyonya raslimali zetu; lakini pia
kulikuwa na mwanya fulani kwa baadhi ya wazawa kufaidi kupitia migongo
ya wawekezaji hao.
Mazingira ya wawekezaji kwa sasa yamebadilika. Sera za uchumi wa
taifa letu hazieleweki na zinazoeleweka hazifuatwi. Serikali inayoimba
wimbo wa uchumi wa soko huria, hivi sasa imetumbukia katika mkakati wa
udikteta unaotishia usalama wa mitaji ya wawekezaji kwa sababu hakuna
umeme wa uhakika.
Aidha, hakuna uhuru kamili wa kuendesha soko huria, hakuna
mazingira sawa ya ushindani na wala hakuna dalili za kukomesha rushwa na
ukiritimba katika shughuli za kiuchumi.
Mzunguko mzima wa shughuli za uwekezaji umejaa rushwa kila hatua na
kutegeana. Mmoja wa wawekezaji wazoefu hapa nchini amenieleza kuwa kila
hatua analazimika kuonana na rais ili aweze kufanya shughuli zake kwa
ufanisi!
Watanzania wameshuhudia mijadala ya ajabu bungeni kuhusiana na
masuala ya uwekezaji na uendeshaji wa shughuli za biashara. Huku katika
upande mmoja bunge likionekana wazi kuingilia wajibu wa serikali na
upande wa pili, bunge likinukia harufu ya udikteta pale lilipofikiria
kutumia jeshi kulazimisha uuzwaji wa mafuta katika vituo vya mafuta.
Hizo ni dalili tosha kuwa “maisha mabaya” kwa kila Mtanzania
yanaipeleka nchi kwenye eneo gumu kiutawala. Unapoona msajili wa vyama
vya siasa akijiingiza kichwakichwa katika kampeini za kubeza maandamano
ya vyama vya siasa, ujue “maisha mabaya” kwa kila Mtanzania yamefika
hata ndani ya ofisi ya msajili wa vyama vya siasa na kumfanya aache
kuwa refa na kuwa mchezaji kamili wa siasa za vyama.
Ni vema tukajiuliza mpaka hapa, ni taasisi gani haijaguswa na
“maisha mabaya” kwa kila Mtanzania. Jeshi la Polisi na Jeshi la Wananchi
yaliingia mapema pale yalipoanza kutumiwa kama matawi ya chama tawala
kutoa matamko elekezi.
Mahakama zilishirikishwa katika semina elekezi za watendaji wa
serikali na kutoa viapo vya kuisaidia katika kukabiliana na wote
wanaohoji kwa nini kuna “maisha mabaya” kwa kila Mtanzania.
Bunge ambalo ni chombo cha wananchi, limegeuka kuwa kama kinyonga.
Mara tunaliona likitoa meno makali, lakini haichukui muda linanywea kama
puto lililoishiwa pumzi.
Panahitajika kauli ya watawala juu ya tulipo sasa, kwa nini tuko
hapa; wamekwama wapi na tuchukue hatua gani kuondoa “maisha mabaya kwa
kila Mtanzania” ambayo yameingia katika kila kaya na maisha ya kila
mmoja. Kunyamaza hakutaondoa chuki ya wananchi.