Kundi la wapiganaji wa Al-Shabab kutoka Somalia limetoa kanda ya video ya propaganda ambayo imemtaja mgombea Urais wa Marekani bwana Donald Trump
Hii imejiri wiki kadha baada ya Trump, anayeongoza kinyang’anyiro cha kutafuta atakayepeperusha bendera ya chama cha Republican, kupendekeza Waislamu wazuiwe kuingia Marekani.
Kundi la al-Shabab, ambalo lina uhusiano na mtandao wa Al-Qaeda, linaelekeza ujumbe kwa Wamarekani weusi, likiwahimiza kusilimu na kushiriki kwenye Jihad au vita vitakatifu.
Kundi hilo linasema kwenye video hiyo kwamba ubaguzi wa rangi, ukatili wa polisi na chuki dhidi ya Waislamu vimesheheni Marekani.
Wasimamizi wa kampeni ya Bw Trump hawajazungumza lolote kuhusu video hiyo.
Miaka ya hivi karibuni, Wasomali-Wamarekani kutoka Minnesota wameripotiwa kwenda Somalia kujiunga na al-Shabab.
Chanzo: BBC

