Shirika la kutetea haki za binaadamu la Amnesty
International limesema kuwa baraza la mpito la Libya lichukue hatua
kuzuia ukiukaji wa haki za binaadamu unaofanywa na wapiganaji
wanaompinga Gaddafi. Katika ripoti yake mpya, shirika hilo linasema
kuwa pamoja na kuwa vikosi vinavyomuunga Gaddafi ndiyo vimehusika na
ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu, wapiganaji wanaompinga pia
wamehusika katika mauaji na kutesa watu.
Mapema,Muammar Gaddafi alisisitiza katika ujumbe kupitia televisheni kuwa wataendelea na mapigano hadi "wapate ushindi".Kwa sasa haijulikani kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 69 yuko wapi.Habari zaidi zinasema kuwa, kiongozi wa baraza
la mpito la Libya Mustafa Abdul Jalil ametoa hotuba yake ya kwanza kwa
taifa mjini Tripoli tangu walipomuondoa Gaddafi, akitoa wito wa kuwa na
taifa lenye msingi wa demokrasia ya kiislamu yenye mfumo wa ''kadri''.
Vikosi vinavyompinga Gaddafi vimesitisha
mashambulio yake dhidi ya mji wa Bani Walid ambao unadhibitiwa na vikosi
vinavyomuunga mkono Gaddafi. Waandishi wa habari wanasema walipata
upinzani mkubwa kinyume na walivyotarajia.

